Baada ya takriban miaka minne ya athari za maradhi ya UVIKO-19, asasi ya kijamii ya Kilimanjaro Dialogue (KDI) nchini Tanzania imeanzisha tena shughuli zake jijini Dar es Salaam kwa kuwakutanisha wadau wa habari ambao katika mazungumzo walikazia umuhimu wa tasnia ya habari katika Afrika kwenda kidigitali zaidi ili kukidhi mahitaji sa kisasa ya kupashana habari na kuongeza ujuzi kwa maisha endelevu na yenye uhakika.
Wakibadilishana mawazo kwenye afla ya kufuturu, kuhusu masuala yanayokabili bara la Afrika kwa hivi sasa, wadau walikubaliana kuwa hakuna mantiki yoyote kwa wamiliki na waajiriwa kwenye tasnia ya habari wala kwa watu wengine kwa ujumla kuhofia kuwa maendeleo ya teknolojia yatasamsababisha mwanadamu kukosa ajira kwa sababu zana zinazotumika ni kazi na akili ya binadamu na kamwe haviwezi kufanya kazi bila binadamu huyo huyo kutia mkono wake. Hata hivyo, wadau hao kutoka kwenye sekta za kijamii, elektronki, ushauri wa habari na asasi za kiraia, walitoa angalizo kuwa pamoja na maendeleo haya, sharti suala ya heshima ya utu wa mtu na haki za kibinadamu vipewe kipaumbele katika nyanja zote za kimaendeleo kiteknolojia, kijamii na kisiasa.
Mitazamo miwili ilijitokeza kwenye mazungumzo hayo. Mshauri wa Habari, Bwana Ezekiel Kamwaga alisema wako viongozi ambao hufanya mambo mazuri pindi waingiapo madarakani. Lakini katika mazingira ya kutokuwepo mfumo mathubuti wa kimawasiliano, wanaishia kukaa juu kwenye viti vyao vya enzi huku wananchi wasijue chochote kinachotendeka, hata kiwe kizuri namna gani. Wako wengine wanaoingia madarakani kupitia chaguzi lakini baada ya kuapishwa hujishughuilisha na kubomoa misingi yote ya demokrasia kwa manufaa yao wenyewe. Wanaishia kutelekeza maslahi ya waliowaweka madarakani ikiwa ni pamoja na kupata habari zilizochambuliwa na za kina. Hapa ndipo suala la tasnia makini linapojitokeza.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Jamii Forums – mojawapo ya asasi za kiraia zinazoibukia katika eneo la Afrika Mashariki (EAC), Kusini mwa Afrika (SADC) na Maziwa Makuu, katika masuala ya utawala bora — Bwana Maxence Melo, alitoa angalizo kuhusu athari za viongozi wanaojiingiza kwenye kampeini za kujitangaza na kueneza propaganda pindi waingiapo madarakani. Alisema viongozi kama hao hupotoka kwa sababu, kama msemo wa Kiswahili usemavyo kwamba “kizuri chajiuza; kibaya chajitembeza”.
Maoni ya Kamwaga na Melo yaliwalenga viongozi wanaoondoka kwenye misingi bora ya utawala na hivyo kuathiri kiwango chao cha utendaji, jambo ambalo linaibua umuhimu wa kuwepo vyombo vya habari makini kama vile Raia Mwema na na waandishi wachunguzi, kama vile Mbarak Islam wa gazeti hilo. Akitilia mkazo juu ya tasnia ya habari kwenda kidigitali zaidi, Bwana Melo alisema Jamii Forums hivi sasa ina uwezo wa kuwafikia watu takriban milioni tano kwa siku , jambo ambalo si jepesi kwa gazeti ya kila siku. Mkurugenzi Hassan Khamis wa Radio Kher amesema wako katika hatua za mwisho za kuanzisha kituo cha televisheni.
Mwenyekiti wa taasisi ya Ishik Medical and Education Foundation (IEMF), Bwana Ismail Yilmaz, alivishauri vyombo vya habari barani Afrika kutoingia mtego wa msimamo hasi wa vyombo wa nchi za Magharibi. “Nina uzoefu wa sehemu nyingi duniani. Kuna kiwango kikubwa cha madabilishano ya mawazo katika Afrika, jambo ambalo ni chanya kwa utawala bora ikilinganishwa na hali halisi katika baadhi ya nchi huko Ulaya. Ukweli huu usipuuzwe,” alisema. Mdhamini wa KDI, Alhaj Habib Miraji, alisema ameshuhudia ukuaji mkubwa wa tasnia ya habari wakati wa awamu zote za serikali ya Tanzania huru kwa kiwango kinachostahiki kuwekewa kumbukumbu.
Katibu Mtendaji wa KDI, Bwana Hassan Mzighani, aliwasihi waalikwa kuwa na ukaribu sana ili kufanikisha malengo ya taasisi huku akiahidi kuandaa fursa zaidi za kubadilishana mawazo kuendana na matukio maalum ya kitaifa, kikanda na kimataifa. Afla hii iliandaliwa katika mgahawa wa Istanbul Reastaurant, unaoendeshwa na Mturuki mmoja, ambaye hapo awali alikwa mwandishi wa habari. Uturuki ni kati ya nchi zinazoongoza duniani kwa kuwatia magerezani waandishi wa habari.